top of page

Watoto wawili wanaosumbuliwa na uzito mkubwa kupita kiasi wamefikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila.

 
Watoto wafikishwa Mloganzila Muhimbili
Watoto wenye uzito mkubwa

 

Ni takribani wiki tatu sasa tangu ripoti za mama wa watoto wenye uzito mkubwa  kuibuka kwenye vyombo vya habari. Mama huyo, aliejulikana kwa jina la Vumilia Elisha, aliomba msaada wa matibabu kwa ajili ya watoto hao, mkubwa akiwa na uzito wa kilogramu 76 na mdogo kilo 62. Baada ya ripoti hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi alisema watoto hao wafikishwe Muhimbili kwa ajili ya matibabu kupitia mfumo wa Rufaa


“Uzito wao ni mkubwa si wa kawaida. Muhimbili tumesikia rai ya mama kuomba msaada, tutakachoomba kikubwa wapewe rufaa ya kuja Dar es Salaam." alisema Prof. Janabi akizungumza na Mwananchi Februari mosi mwaka huu.


“Kwa kuwa mwaka moja uliopita Hospitali ya Taifa Muhimbili ilichaguliwa moja ya zile nne barani Afrika kushungulikia mambo ya uzito mkubwa ‘lipid clinic’ zinazoshughulikia tatizo la mafuta na tunafanya kazi na wenzetu wa Uingereza, sisi ni moja ya kituo cha hizi kliniki barani Afrika,” amesema Janabi.


Mchakato wa matibabu


Kuhusiana na mchakato wa matibabu Prof. Janabi alisema “Kuna vipimo vingi tutawafanyia, ni mapema kusema mpaka pale watakapokuwa wamefika. Kubwa kwetu ni lazima tuanze uchunguzi na kama ni tiba tuanze mapema kwa kuwa uzito unakuja na magonjwa mengi ya moyo, figo, kisukari, kiharusi itakuwa ni muhimu sana kuwasaidia,”


“Wenyewe kwa wenyewe wanaitana bonge inaweza kuwaathiri kisaikolojia,” hivyo watahakikisha wanapata tiba ya kisaikolojia wao na wazazi wao kwa kipindi watakachokuwa wakiendelea na matibabu.





“Matatizo haya yanaweza kuwa tofauti, tutawachunguza na tukipata majibu tutaanza tiba. Mara nyingi husababishwa na homoni za madini joto. Pia inaweza kuwa matatizo ya kurithi ya vinasaba ni muhimu wakafika mapema kwa ajili ya uchunguzi kwa kuwa wanaweza kuwa na shida ya homoni au vichocheo ambavyo vinaweza kusababisha changamoto nyingine zikaleta madhara kwenye moyo na mishipa ya damu" alisema Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo Mloganzila, anayehusika na matibabu ya magonjwa ya matatizo ya mafuta kwenye damu, Dk. Rosemary Minja.



Historia ya watoto hao


Imani (6) na Gloria Joseph (4) wamezaliwa kwenye familia ya watoto wanne, wanauzito kuliko umri walionao hali ambayo ni hatarishi kwa afya zao na kwa mujibu wa mtaalam wa Afya ya Jamii, Dk. Ali Mazige, "Mtoto mwenye umri wa miaka minne anapaswa kuwa na uzito wa kilogramu 16 na mwenye umri wa miaka sita anapaswa kuwa na uzito wa kilogramu 22 hii haijalishi anaishi Ulaya au Tanzania hii ndio kanuni ya afya."


Mama wa watoto hao ameeleza kuwa watoto walizaliwa na kilo 3 lakini walianza kuongezeka uzito kwa kasi kila mwezi, kwa mfano Imani aliongezeka kilo 7 ndani ya miezi miwili ndipo manesi wa kliniki ya mama na mtoto walipomshauri amnyonyeshe kwa ratiba jambo ambalo amesema halikusaidia kitu, ndipo alipoamua kuwapeleka hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ambapo Imani aligundulika kuwa na tatizo la homoni.


Kwa upande wa Gloria historia ikajirudia kuzaliwa na kilo 3 na uzito kuendelea kuongezeka kwa kasi. Mama alijaribu kuwapa mlo kamili 'diet' kama alivyoshauriwa hospitalini lakini alishindwa kuendelea kwa sababu ya ugumu wa maisha na kuanza kuwapa kile kinachopatikana.


Dk. Julieth Kabengula, daktari bingwa wa watoto kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, akifanya mahojiano na gazeti la Mwananchi amesema kuwa changamoto ya uzito wa kupitiliza kunasababishwa na vitu vingi sio suala la homoni peke yake. Aliongeza kuwa kama tatizo ni homoni linaweza kurekebishika, lakini pia linaweza kuwa limeleta matatizo mengine ya kiafya ambayo yanahitaji uchunguzi wa kitaalamu zaidi.


 

Taarifa bora, Afya bora ∣ Dawacheck®

bottom of page