top of page

Matibabu na kinga dhidi ya minyoo katika nyama ya nguruwe.


Picha ya nyama mbichi ya nguruwe

Maambukizi ya minyoo ya nguruwe kwenye mfumo mkuu wa mishipa ya fahamu ni chanzo kikuu cha kifafa duniani kote. Neurocysticercosis (kwa lugha ya kitaalamu) ni maambukizi ya vimelea, yanayozuilika ambayo huathiri mfumo mkuu wa neva ugonjwa ambao husababishwa na minyoo ya nguruwe ijulikanayo kama Taenia solium. Binadamu huambukizwa baada ya kula chakula kisichoiva vizuri, hasa nyama ya nguruwe, au maji yaliyo na mayai ya minyoo, au kupitia mazoea duni ya usafi.


Kama maambukizi ya minyoo hii ya nguruwe kwenye utumbo mkubwa hayatatibiwa, mtu anaweza kupata ugonjwa mbaya zaidi ujulikanao kama cysticercosis pale ambapo mayai ya minyoo ya T. solium yanapoingia kwenye tishu za mwili. Wakati mayai haya yanapojikusanya kwenye mfumo mkuu wa neva, misuli, ngozi na macho, husababisha neurocysticercosis - hali hii ya ugonjwa ni chanzo cha kifafa kwa watu wengi duniani kote.


Matibabu yanajikita katika kuondoa minyoo na kudhibiti dalili kwa kudhibiti kifafa, uvimbe, na shinikizo la juu la damu kwenye ubongo. Aina sahihi ya matibabu pia itategemea nafasi, ukubwa, wingi, na ukomavu wa minyoo.


Matibabu


Baada ya kuchunguza dalili za mtu na kiwango cha maambukizi, daktari anaweza kutumia tiba ya kuzuia minyoo na kupunguza uvimbe. Katika baadhi ya matukio, upasuaji unahitajika kuondoa vivimbe.


Kwa watu wenye dalili na vivimbe vingi vilivyo hai, madaktari wanaweza kutumia dawa ya minyoo. Hata hivyo, njia hii haifai kwa watu wenye vivimbe/minyoo iliokufa. Daktari anaweza pia kutoa dawa za kupunguza uvimbe na tiba ya kuzuia kifafa ili kudhibiti kifafa.


Katika maeneo ambapo neurocysticercosis hutokea mara kwa mara, wataalamu wa mifugo wanaweza kutibu nguruwe kwa chanjo na dawa za kuzuia minyoo ili kusimamisha mzunguko wa ugonjwa huu.


Muda wa kupona unategemea mambo mbalimbali ya mtu binafsi kama umri, kiwango cha maambukizi na uwepo wa magonjwa mengine.


Kuondoa minyoo ya aina hii, mara nyingi matibabu hufanyika kwa kutumia dawa zilizoagizwa na daktari wako. Dawa za kutibu ugonjwa huu (taeniasis) ni pamoja na praziquantel na albendazole.


Dawa hizi ni za kundi la dawa za minyoo (antihelmintics), ambazo zinaua vimelea vya minyoo na mayai yao. Katika hali nyingi, dawa hizi hutolewa kwa dozi moja. Zinaweza kuchukua wiki chache kumaliza maambukizi kabisa. Minyoo itatolewa kama taka.


Madhara ya kawaida yanayohusishwa na dawa hizi ni pamoja na kizunguzungu na kuchafuka tumbo.

 

KINGA


Ili kujikinga na maambukizi ya minyoo ya nguruwe aina ya Taenia solium, ni muhimu kupika nyama ya nguruwe kwa usahihi. Hapa kuna maelekezo ya jinsi ya kupika nyama ya nguruwe ili iwe salama kwa kula:


  • Kwa vipande vikubwa vya nyama ya nguruwe: Pika hadi joto la ndani ya nyama lifikie angalau nyuzi joto 63°C (145°F) kama ilivyopimwa na kipima joto cha chakula kilichowekwa sehemu nene zaidi ya nyama, fanya hivi kwa dakika 10 au zaidi ili kuua vimelea vyote. Baada ya kufikia joto hili, acha nyama ipumzike kwa dakika 3 kabla ya kuikata au kula, hili husaidia kuua vimelea vilivyo jificha ndani ya nyama.

  • Kwa nyama ya nguruwe iliyosagwa: Pika hadi joto la ndani lifikie angalau nyuzi joto 71°C (160°F). Nyama ya nguruwe iliyosagwa haitaji muda wa kupumzika baada ya kupika.

Kutumia kipima joto cha chakula ni njia bora ya kuhakikisha kwamba nyama ya nguruwe imefikia joto linalohitajika kuua minyoo yoyote. Kumbuka, nyama haipaswi kuwa na sehemu zenye rangi ya pinki wakati imepikwa kabisa. Daima fanya usafi mzuri kwa kunawa mikono na sehemu zilizoguswa na nyama mbichi ya nguruwe.


 

Taarifa bora, Afya bora ∣ Dawacheck©

 

bottom of page