top of page

Hizi hapa sababu zinazopelekea mimba kuharibika


Mimba kuharibika

Kuharibika kwa mimba ni kupoteza kwa ujauzito ghafla kabla ya wiki ya 20. Takribani 10% hadi 20% ya mimba huharibika. Lakini idadi halisi ni kubwa zaidi. Hii ni kwa sababu mimba nyingi huharibika mapema, kabla ya watu kutambua kuwa wana mimba. Hivyo mimba nyingi huharibika ndani ya wiki 13 za kwanza.


Kuharibika kwa mimba hutokea kwa sababu ukuaji wa mtoto ambaye hajazaliwa hakuendelei vizuri au kiinitete kiliacha kukua kabisa.


Aina za ujauzito unaoharibika


Missed miscarriage: Umeupoteza ujauzito bila ufahamu wako. Hakuna dalili, lakini kipimo/ultrasound inathibitisha kuwa hakuna mapigo ya moyo.


Complete miscarriage: Umepoteza ujauzito na kizazi chako ni tupu. Umeona damu na ukapitisha mabaki ya kiinitete. Mtoa huduma wako anaweza kuthibitisha kwa kipimo/ultrasound.


Recurrent miscarriage: Mimba imeharibika mara tatu mfululizo bila kuzaliwa. Inaathiri takribani 1% ya wanandoa.


Threatened miscarriage: Shingo yako ya kizazi inabaki imefungwa, lakini unatokwa na damu na unahisi maumivu ya tumbo. Unaendelea na ujauzito bila shida yoyote. Mtoa huduma wako anaweza kukufuatilia kwa karibu zaidi kwa mudauliyobaki wa ujauzito wako.


Inevitable miscarriage: Unatokwa na damu, unahisi maumivu na shingo yako ya kizazi imeanza kufunguka (kupanuka). Unaweza kuvuja maji ya uzazi. Kuna uwezekano mkubwa wa mimba kuharibika.


Dalili zinaweza kujumuisha:

·       Kutokwa na damu kutoka ukeni kukiambatana na maumivu au bila maumivu, pamoja na kutokwa na damu nyepesi inayotia doa.

·       Maumivu au kufinyana katika eneo la tumbo au mgongo wa chini. (kawaida mbaya kuliko maumivu ya hedhi)

·       Maji au vipande vya mabaki kutoka ukeni.

·       Mapigo ya moyo haraka.


Ikiwa mabaki yamekutoka ukeni, weka kwenye chombo safi. Kisha, upeleke kwenye ofisi ya mtaalamu wako wa afya au hospitali. Maabara inaweza kuchunguza mabaki hayo ili kuangalia dalili za kuharibika mimba. Kumbuka kuwa watu wengi wajawazito ambao wana doa au kutokwa na damu ukeni katika miezi 3 ya kwanza huendelea kuwa na ujauzito wenye mzuri. Lakini fika katika kituo cha afya ikiwa utatokwa na damu nyingi au kunatokea na maumivu ya tumbo ya kufinyana."

 

Sababu zinazopelekea mimba kuharibika


Matatizo ya vinasaba husababisha takribani 50% ya mimba zote zinazoharibika, sababu zingine ni pamoja na

• Maambukizo ya magonjwa.

• Kutofautiana kwa homoni.

• Kupandikizwa vibaya kwa yai lililorutubishwa kwenye utando wa kizazi.

• Umri wako.

• Matatizo ya kizazi.

• Shingo ya kizazi isiyo imara (shingo yako ya kizazi huanza kufunguka mapema katika ujauzito).

• Mambo ya mtindo wa maisha kama vile kuvuta sigara, kunywa pombe au kutumia dawa za kulevya.

• Matatizo ya mfumo wa kinga mwili kama lupus.

• Ugonjwa mkali wa figo.

• Ugonjwa wa moyo wa kuzaliwa nao.

• Kisukari ambacho hakijadhibitiwa.

• Ugonjwa wa tezi ya thyroid.

• Mionzi.

• Dawa, kama vile dawa ya chunusi isotretinoin

• Utapia mlo

• Unene (uzito mkubwa)






Hakuna ushahidi wa kisayansi kwamba msongo, mazoezi, ngono au matumizi marefu ya vidonge vya kuzuia mimba husababisha kuharibika kwa mimba. Hali yako iweje, ni muhimu usijilaumu kwa kuharibika kwa mimba.

 

Vihatarishi vya mimba kuharibika ni pamoja na:


Umri wako: Utafiti unaonyesha kuwa hatari ya mimba kuharibika ni 12% hadi 15% kwa watu wenye umri wa miaka 20 na inapanda hadi karibu 25% kwa watu wenye umri wa miaka 40. Mimba nyingi zinazoharibika kwa sababu ya umri hutokea kwa sababu ya hitilafu ya kijenetiki.

 • Kuharibika kwa mimba moja: Una nafasi ya 25% ya kupata mimba nyingine iliyoharibika ikiwa umeshawahi.

Hali za kiafya: Hali fulani za kiafya kama kisukari kisichodhibitiwa, maambukizi au matatizo na kizazi au shingo ya kizazi huongeza nafasi yako ya mimba kuharibika.


Uchunguzi na Vipimo 


Jinsi gani kuharibika kwa mimba kunagunduliwa?


Mhudumu wako wa huduma ya ujauzito atafanya kipimo cha ultrasound ili kuthibitisha kuharibika kwa mimba. Vipimo hivi huchunguza mapigo ya moyo wa kiumbe au uwepo wa kifuko cha yai (moja ya muundo wa kwanza wa kiumbe ambao mhudumu wako anaweza kuona kwa ultrasound). Pia unaweza kupata kipimo cha damu ili kupima homoni ya koriogonadotropini ya binadamu (hCG), homoni inayozalishwa na kondo la nyuma. Viwango vya chini vya hCG vinaweza kuthibitisha.


Usimamizi na Matibabu 


Ikiwa utapoteza ujauzito, mtoto lazima atolewe kwenye mfuko wa uzazi. Ikiwa sehemu yoyote ya ujauzito itabaki ndani ya mwili wako, unaweza kupata maambukizi, kutokwa damu, au shida nyingine.

Ikiwa kuharibika kwa mimba kumekamilika na mfuko wa uzazi umetoa mabaki yote ya kiinitete, basi kawaida hakuna matibabu zaidi yanayohitajika. Mhudumu wako atafanya kipimo cha ultrasound kuhakikisha hakuna kitu kilichobaki kwenye mfuko wako wa uzazi.

Ikiwa mwili wako hautaondoa mabaki yote au ukaanza kutokwa damu, mhudumu wako atapendekeza kuondoa mabaki kwa kutumia dawa au upasuaji.


Matibabu Bila Upasuaji 

Mhudumu wako anaweza kupendekeza kusubiri kuona kama mimba itatoka yenyewe. Hili hufanyika pindi mimba inapoharibika bila ufahamu wako  Unaweza kusubiri siku kadhaa hadi mimba iliyoharibika ianze kutoka.. Ikiwa kusubiri si salama au unataka kuondoa mabaki haraka iwezekanavyo, wanaweza kupendekeza kutumia dawa inayosaidia mfuko wako wa uzazi kutoa mimba. Haya yanawezekana kama mimba imeharibika kabla ya wiki 10 za ujauzito.


Ikiwa kuharibika kwa mimba hakujathibitishwa, lakini ulikuwa na dalili za kuharibika kwa mimba, mhudumu wako anaweza kuagiza kupumzika kitandani kwa siku kadhaa. Unaweza kulazwa hospitalini kwa uchunguzi. Utokaji damu ukikoma unaweza kuendelea na shughuli zako za kawaida. Ikiwa mlango wa kizazi wako umefunguka, wanaweza kugundua kuwa mlango wa kizazi umelegea, na wanaweza kufanya upasuaji wa kufunga mlango wako wa kizazi (cervical cerclage).


Matibabu ya mimba iliyoharibika

Matibabu Kwa Upasuaji


Matibabu yanahusisha kufungua njia ya uzazi  na kutumia vifaa maalum kutoa mabaki ndani ya mfuko wako wa uzazi au ikiwa unavuja damu kwa wingi. Upasuaji pia unaweza kuwa njia pekee ikiwa ujauzito wako umepita wiki 10 za ujauzito. Katika taratibu hizi, mlango wa kizazi wako hufunguliwa, na mabaki yoyote yanayohusiana na ujauzito huondolewa au kunyonywa kwa polepole kutoka kwenye mfuko wako wa uzazi. Matibabu haya hufanyika hospitalini ukiwa katika nusu kaputi.


Ni vipimo gani ninavyohitaji baada ya mimba kuharibika mara kwa mara?


Utafanyiwa vipimo vya damu au vya kijenetiki ikiwa mimba itaharibika zaidi ya mara tatu mfululizo (mimba kuharibika mara kwa mara). Vipimo hivi ni kama ifuatavyo:


Vipimo vya kijenetiki: Wewe na mwenzi wako mnaweza kupima damu, ili kuchunguza kama kuna kasoro za vinasaba. Ikiwa mabaki kutoka kwenye mimba iliyoharibika yanapatikana, mtoa huduma wako anaweza kupima mabaki hayo.

Vipimo vya damu: Unaweza kupima damu ili kuchunguza kama kuna hali za kinga au homoni zinazosababisha mimba kuharibika.


Nawezaje kuzuia mimba kuharibika?


Haiwezekani kuzuia mimba kuharibika. Ikiwa mimba itaharibika, sio kwa sababu ulifanya kitu cha kusababisha hivyo. Lakini unaweza kufanya mambo yanayoweza kupunguza uwezekano wa mimba kuharibika.


Baadhi ya mifano ya njia za kujitunza ili kupiunguza uwezekano wa kupoteza ujauzito ni pamoja na:

• Kuhudhuria kliniki kila wakati kabla ya kujifungua.

• Kudumisha uzito unaofaa kwako.

• Kuepuka mambo yanayoweza kusababisha mimba kuharibika kama kunywa pombe na kuvuta sigara.

• Kunywa vitamini za ujauzito.

• Kufanya mazoezi ya kawaida na kula lishe bora.


Je! Ninaweza kushika mimba baada ya kupata tatizo la mimba kuharibika?

 

Ndiyo. Asilimia 87 ya watu ambao wamepata tatizo hili hupata mimba na kujifungua kwa kawaida baadaye. Mimba kuharibika hakumaanishi kuwa una shida ya uzazi. Kumbuka, mimba nyingi zinaharibika kwa sababu za kijenetiki, sio kwa sababu ya kitu ulichofanya.


Ni lini ninaweza kushika mimba baada ya kupata mimba kuharibika?


Uamuzi wa lini unapaswa kuanza kujaribu kushika mimba tena ni kati yako na mtoa huduma wako wa afya. Watu wengi wanaweza kushika mimba tena baada ya kupata hedhi moja ya “kawaida”. Pata muda wa kupona kimwili na kihisia na usijilaumu kwa kupoteza ujauzito. Omboleza, na ikiwa mimba zimeharibika mara tatu mfululizo, muulize mtoa huduma wako kuhusu kufanya vipimo ili kubaini sababu ya msingi.


 

Taarifa bora, Afya bora ∣ Dawacheck©

 

 

bottom of page