top of page

Kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu miongoni mwa magonjwa yaliomkabiri Lowasa

 
Picha ya utumbo mdogo na utumbo mpana

Februari 10 Tanzania iliamka na taarifa za kifo cha aliekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Edward Lowasa afariki dunia, wakati akiendelea na matibu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI). Mh. Lowasa ameugua kwa takribani miaka miwili akipatiwa matibabu nchini Afrika Kusini na Tanzania kabla umauti kumkuta.


Amefariki leo akipatiwa matibabu kwa ugonjwa wa utumbo kujikunja, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu. Hayati Edward Lowassa ameugua kwa muda mrefu na amekuwa akipatiwa matibabu tangu Januari 14, 2022 JKCI na baadaye akapelekwa kwa matibabu zaidi nchini Afrika Kusini na kurejea tena JKCI,” alisema Dk Philip Mpango, Makamu wa Raisi, akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia televisheni ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).


Utumbo kujikunja


Sehemu ya utumbo mkubwa au mdogo inaweza kuzunguka na kujikunja kutokana na matatizo ya muundo wa utumbo mpana, kufunga choo, na masuala mengine ya afya. Wazee kati ya umri wa miaka 50 na 80 wako katika hatari zaidi ya utumbo kujikunja. Pia ni kawaida kwa watoto wachanga waliozaliwa na tatizo la utumbo uliozunguka vibaya. Hali hii inaweza kukata usambazaji wa damu kwenye eneo husika la utumbo, na kusababisha dalili kama vile maumivu makali, kinyesi chenye damu, kuoza kwa utumbo, kutoboka utumbo na kuziba kwa utumbo kunakopelekea chakula kushindwa kupita. Ni dharura ya kitabibu inayohitaji upasuaji.

Mkunjo kwenye utumbo mpana (sigmoid volvulus)

Dalili za utumbo uliojikunja


Dalili za utumbo kujikunja hutokea taratibu na kuzidi kuwa mbaya, tumbo huanza na kusokota, lakini maumivu hatimaye yanakuwa hayavumiliki. Dalili zingine ni kama:-


  • Kuvimba kwa tumbo

  • Uchungu wa tumbo

  • Kutapika

  • Damu katika kinyesi

  • Kufunga choo


Visababishi


Sababu za utumbo kujikunja hazijulikani kwa uhakika kabisa. Inatokea hasa kwa watu wazee kati ya umri wa miaka 60 na 80. Mara nyingi huathiri watu wanaoishi na magonjwa ya mishipa ya fahamu. Hutokea zaidi kwa watu wanaoishi kwa kutumia muda mwingi kitandani.


Matibabu


Matibabu kwa upasuaji yatategemea kiwango cha jeraha la utumbo ili kusaidia kuamua ikiwa kuunganisha tena utumbo au upasuaji unahitajika. Kawaida, ikiwa sehemu ya utumbo uliooza sio kubwa, kumekuwa na mafanikio makubwa katika kuunganisha tena utumbo bila upasuaji.


Hivyo kulingana na hali ya mgonjwa njia kadhaa zisizo za upasuaji zinaweza kutumika, njia hizo ni kama vile "sigmoidoscopy" ambapo daktari ataweka bomba laini (au sigmoidoscope) kupitia njia ya haja kubwa na kuingia sehemu ya chini ya utumbo mpana. Kiasi kidogo cha hewa kinapigwa ndani ya utumbo ili kuufungua. Hii kawaida inatosha kunyoosha utumbo, tiba hii humsaidia pia daktari kufanya tathmini kama mgonjwa atahitaji upasuaji. Uwezekano wa utumbo kurudia tena kujikunja mahali hapo ni mkubwa sana. Daktari wako anaweza kupendekeza upasuaji kama suluhisho la kudumu.



matibabu ya utumbo uliojikunja
Kifaa cha kunyoosha utumbo uliojikunja

Utaratibu unaofanana na sigmoidoscopy, yaani colonoscopy, unaweza kutumika kwa matibabu ya utumbo uliojikunja mwanzoni mwa utumbo mpana. Lakini uwezekano wa kujikunja tena ni mkubwa ndio maana kesi nyingi katika eneo hili zinahitaji upasuaji.


Aina za upasuaji


Njia ya upasuaji ni njia nzuri zaidi kwa ajili ya kuzuia tatizo hili kujirudia tena. Njia hizo ni kama ifuatavyo


Colectomy: Hii ni upasuaji unaotoa sehemu au sehemu yote ya utumbo mpana. Kwa mkunjo kwenye sehemu ya chini ya utumbo mpana, daktari atatoa sehemu iliyohusika ya utumbo wako. Kisha, wataunganisha sehemu mbili zenye afya. Uwezekano wa mkunjo kurudi baada ya upasuaji huu ni mdogo sana.


Colostomy: Kama colectomy, upasuaji huu unahusisha kutoa sehemu iliyojikunja ya utumbo wa chini. Kwa colostomy, badala ya kuunganisha sehemu mbili za utumbo pamoja, upande mmoja wa tundu unaunganishwa na mfuko wa colostomy ili kuondoa taka mwili.


Ikiwa unaonyesha dalili za maambukizo au dalili zingine kali kutokana na utumbo uliojikunja, daktari anaweza kufanya kinachoitwa Hartmann procedure. Ni sawa na colostomy, isipokuwa inaweza kutolewa baada ya miezi 3 hadi 6 ikiwa hali itatengemaa.


Cecostomy: Sehemu ya utumbo mpana iliojikunja hunyooshwa. Kisha, daktari anaweka bomba nyembamba kwenye eneo hilo kupitia tundu dogo kwenye tumbo. Bomba husaidia kuondoa taka na kuunganisha utumbo na ukuta wa ndani wa tumbo. Watu hufanyiwa cecostomy ikiwa hawana afya ya kutosha kufanyiwa upasuaji mwingine. Uwezekano wa kupata maambukizo ni mkubwa, lakini utumbo labda hautajikunja tena.


Cecopexy: Madaktari watakunjua sehemu ya utumbo iliojikunja na kuushona kwenye ukuta wa ndani wa tumbo. Baada ya utaratibu huu, kuna uwezekano mkubwa kwamba eneo lile lile litazunguka tena. Kwa hivyo, kawaida hufanyiwa watu wenye hali dhaifu kiafya.


 

Taarifa bora, Afya bora ∣ Dawacheck©



bottom of page